makala sahili

LoGo

Kazi za viinilishe mwilini

Alphonse S. Mahuyemba


Functions of nutrients in the body
Vitamini A
Mboga za majani zina kiini-ghafi cha vitamin A (ß-carotene) ambacho wakati wa mumeng’enyo wa chakula hubadilishwa kuwa vitamnini A kamili.
Kazi za Vitamini A:
Vitamini A ni muhimu katika kudumisha afya ya chembechembe-tete za ngozi.
Huimarisha nguvu ya macho kuona; na hasa penye mazingira ya mwanga hafifu.
Huzuia kudumaa katika makuzi; huchangia katika kasi bora ya ukuaji wa viumbe wachanga (watoto).
Huzuia mabakabaka (vibarango) yatokanayo na ukosefu wa vitamin A.
Upungufu/ukosefu wa vitamini A husababisha kudumaa, ukavu wa ngozi, vibarango na upofu katika mwanga hafifu.

Vitamini B1 (thiamine)
Hii ni vitamini muhimu isaidiayo mwili katika kumeng’enya chakula cha wanga (hamilojo).
Ukosefu wa vitamnini B1 husababisha dalili za mapungufu katika utendaji wa neva za fahamu (beriberi).

Vitamini B2 (riboflavin)
Vitamini B2 ina mchango katika mwili kumeng’enya protini (utomwili).
Ukosefu wa vitamini B2 husababisha magonjwa ya ngozi na kufanya vijeraha katika ngozi kutopona upesi.

Vitamini B6 (pyridoxine)
Vitamini B6 ni muhimu katika umeng’enyaji wa viini-tete vya protini (amino acids).
Upungufu wa vitamini B6 husababisha matatizo katika mfumo wa neva za fahamu. Kwa binadamu hali hiyo huambatana na mavune (uchovu), mifadhaiko, kung’aka (nafsini) kusiko na sababu, kukosa usingizi, pia panaweza kuwa na matatizo katika kutembea.

Vitamini B12 (cobolamine)
Vitamini hii huungana na madini ya koboti (cobalt) katika utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu: Upungufu wa vitamin B12 husababisha upungufu wa damu.

Vitamini E (tocopherol)
Vitamini E ni muhimu katika kuimarisha afya ya ngozi, na huboresha mzunguko wa damu mwilini. Vitamini hii pia huboresha na kuimarisha kinga ya mwili na afya ya uzazi.

Vitamini D (calciferol)
Binadamu hujitengenezea vitamnin D chini ya ngozi yake maadam tu awe ameota jua la asubuhi lisilo na joto kali; na awe pia amekula mboga za majani.
Umuhimu wa vitamini D umo katika kuuwezesha mwili kutumia madini ya kalsiumu na fosforasi; hayo ni madini ambayo mwili huyatumia kujitengenezea na kuimarisha mifupa: Vitamini D huongeza kasi ya madini hayo kuchukuliwa kwenda mwilini kutoka kwenye utumbo.
Upungufu wa vitamin D husababisha miguu na mifupa mingine kupinda (matege) kwa watoto wadogo na wanyama wengine ambao wangali wanakua.

Vitamini K
Vitamini K inahusika katika kutengeneza kisababisho cha damu kuganda (prothrombin). Upungufu wa vitamin hii unaweza kuwa na dalili za upungufu wa damu, ongezeko la utokwaji damu na kasi ndogo ya damu kuganda. Mboga za majani ni chanzo kizuri cha vitamini hii.

MADINI
Madini ya Chuma (Fe)
Madini ya chuma (Fe) ni sehemu muhimu ya chembechembe nyekundu za damu: Mwili uwapo na madini ya chuma ya kutosha huimarisha utengenezaji wa damu. Upatikanaji wa madini ya chuma mwilini huimarisha na kuboresha utendaji kazi wa mfumo wa neva za fahamu (taamuli).
Upungufu/ukosefu wa madini ya chuma mwilini husababisha upungufu wa damu. Upungufu huo pia huambatana na dalili za mavune (uchovu wa mwili), uchovu wa misuli, upungufu wa usitahimilivu (stamina); ugumu wa kujifunza kizingativu na mapungufu katika uwezo wa kutatua matatizo (problem solving disabilities).

Madini ya Kalsiumu (Ca)
Madini ya kalsiumu (Ca) huimarisha mifupa na meno. Kalsiumu ikiwa pamoja na fosforasi hudumisha ugumu na uimara wa mifupa na meno. Mwili hujitunzia akiba ya kalsiumu yake kwenye mifupa. Akiba hiyo huweza kutumika kwa uwezesho wa vitamin D pawapo na mahitaji ya ziada mwilini kwa mfano wakati wa kunyonyesha.
Vile vile kazi nyingine ya kalsiumu ni kuwezesha damu kuganda kirahisi. Pia, kalsiumu, ni muhimu katika utendaji kazi wa neva za fahamu na unyumbulifu wa misuli mwilini.

Madini ya Fosforasi (P)
Fosforasi (P) ikiwa na kalsiumu huimarisha mifupa na meno. Mifupa ni kiungo kitunzacho akiba ya fosforasi na kalsiumu mwilini.
Kuwapo kwa vitamin D mwilini huboresha ‘ufyonzaji’ wa kalsiumu na fosforasi kutoka kwenye utumbo na kuingizwa kwenye mfumo wa uimarishaji wa afya ya mifupa na meno. Patokeapo mahitaji ya ziada ya madini hayo; vitamini D huwezesha utoaji wa homoni (parathyroid hormone) ambayo hurahisisha upatikanaji wa kalsiumu na fosforasi kutoka kwenye akiba yake (katika mifupa) mwilini.

Utomwili (Protein)
Kiinilishe cha utomwili (protein) ni malighafi muhimu katika kujenga mwili wa kiumbe hai. Protini iundayo sehemu nyingi za mwili (hasa misuli) hutokana na viinilishe-tete vya aina mbalimbali za tindikali (Amino acids). Kutokana na aina hizo za tindikali hutengenezwa aina mbalimbali za protini ambazo huunda misuli, vitendanishi katika mumeng’enyo (enzymes), homoni, vilainisho na kadhalika.
- Alphonse Shija MAHUYEMBA

Soma zaidi hapa (kitabu) Vitabu sahili

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Taarifa zilizo katika mtandao huu hazilengi kuwa mbadala wa taarifa rasmi kutoka katika vyombo vyenye mamlaka kama, daktari au mtoa huduma ya afya. Au sekta yoyote rasmi. Taarifa na habari hizi ni kwa ajili ya ujuzi tu.