makala sahili

LoGo

Makala za kiupembuzi zilizoandikwa na waandishi makini. Jiandae kupata madini ambayo yatabadilisha au kukufikirisha upya kabisa. Na kama iwapo utapenda kuwa mmoja wa waandishi hawa usisite.

GO_HOME

Makala Zilizochapishwa

Naam zilizopata kuandikwa; Kufungua bofya 'soma zaidi' iliyo kushoto

Mwandishi wa biblia ni nani ?
Biblia kama inavyotumika hivi sasa ni Maandiko Matakatifu. Ni Maktaba ya aina ya pekee inayohifadhiwa katika kitabu kimoja. Neno biblia linatokana na neno la kigiriki ambalo ni wingi wa Biblos. Kila kijitabu (Biblos) kilichoandikwa kilitumika pekee pamoja na kuhusishwa na vijitabu (Biblia) vingine vilivyosimulia mambo Matakatifu. Baadhi ya vijitabu hivyo baadaye viliteuliwa na kuhifadhiwa kwa pamoja kama kitabu kimoja na hiyo ndiyo biblia itumikayo katika zama hizi.

Maandiko matakatifu husimulia habari za aina aina. Sehemu ya kwanza Biblia au Agano la Kale husimulia mambo ya historia, mafunzo ya msingi, Sanaa ya kishairi na mambo ya unabii. Katika sehemu ya pili yaani Agano jipya husimulia habari njema au injili na Matendo ya Mitume – ambayo pia ni mambo ya kihistoria. Pia mna nyaraka mbali mbali za upashanaji habari njema na mambo ya Unabii yako kwenye kijitabu cha Ufunuo.

Masimulizi katika Biblia yenye mtazamo wa maudhui ya historia husimulia hadi matukio ya kabla ya nyakati (Mwanzo); Kitabu kinachotaja ya mwanzo kabla ya kuwepo mwanadamu; uandishi wake ni wa aliyekuwapo kabla ya ‘wakati’. Aliyekuwapo kabla ya wakati ni mungu (Mwa. 1:1–3; Yah. I:1,2). Maandiko Matakatifu yaliandikwa kwa uongozi wa Roho Mtakatifu wa Mungu. Wanadamu walioshika kalamu na kuyaweka penye karatasi walifanya hivyo kwa kuongozwa na Mungu (2 Tim. 2:16,17).

Hapo juu pametaja kwamba vijitabu mbalimbali viliandikwa na baadaye baadhi yake viliteuliwa na kuhifadhiwa kama Biblia ilivyo leo. Katika biblia hakuna panapoelezea wazi ni vingapi viliandikwa. Ni historia ya elimu-dunia tu ndiyo huelezea ya kuwa mamia kadhaa ya vijitabu aina hiyo viliandikwa. Vijitabu visivyozidi mia ndivyo vilitumika katika uhifadhi wa maktaba hiyo maalumu na kutunzwa katika kitabu kimoja kiitwachi biblia. Biblia itumikayo na Waprotestanti inavyo vijitabu 66, na madhehebu ya katoliki wana vijitabu vipatavyo 72 katika Biblia waitumiayo.

Matumizi ya vijitabu vya maandiko matakatifu katika kuelezea habari za Mungu yalianza karne nyingi kabla ya kuzaliwa Kristo (K.K). Pamoja na kutokujulikana wazi ni lini hasa vijitabu vya agano la kale vilikusanywa na kuhifadhiwa kama kitabu kimoja; inafahamika kuwa tafsiri ya watafsiri 70 ilikamilishwa miaka mia mbili kabla ya kuzaliwa Kristo (200 K.K). Wakatafsiri Kiebrania katika Kigiriki. Yasemekana watafsiri hao 70 wakifanya kazi kila mmoja lwake (kivyake), walikamilisha kazi iliyofanana sana ilipolinganishwa. Hapo hata kazi hiyo ya kutafsiri ilionyesha kuwa ilihusu kazi iliyoongozwa na Mungu.

Uandishi wa vijitabu vilivyo katika Agano Jipya ulianza mnamo miaka ipatayo kumi hivi baada ya kufa na kufufuka Yesu Kristo. Uandishi wa vijitabu hivi ulikamilika mnamo karne ya kwanza baada ya kuzaliwa Kristo (96 B.K.). Kwa ujumla wake, uandishi wa vijitabu vyote vilivyomo katika biblia ulikuwa nyakati mbalimbali na ulikamilishwa katika kipindi cha zaidi ya karne 16. Ni kazi iliyowahusisha wasika kalamu wapatao 40 kuikamilisha, Mwanzo – Ufunuo. Inakisiwa kijitabu cha Mwanzo Musa alikikamilisha mnamo mwaka 1513 K.K naye Yohane akakikamilisha kijitabu cha ufunuo mnamo mwaka 96 B.K.

Viongozi wa Kanisa mara nyingi wanashauri ilivyo muhimu kujisomea neno la mungu kwa ustawi wa roho. Si hivyo tu, bali pia wameonya ilivyo muhimu kusoma Maandiko Matakatifu na kupata ufafanuzi wake sahihi. Kitabu hicho ni tofauti na vitabu vya elimu dunia. Baadhi ya watu mashuhuri wa dunia iliwahi kuwabidi kutaka msaada kuyaelewa maandiko. Mfano ni yule mkurugenzi maarufu wa hazina ya malkia wa Ethiopia (Mate. 8:26-38). Hali kadhalika siyo rahisi kwa msomaji kuelewa kutokupunguza au kuongeza katika ‘kitabu hiki’ (Yoh. 22:18’ Kumb. 4:2, 12:32; Dan.). Je washika kalamu haowalisema juu ya walichokiandika juu ya vijitabu vyao tu ? Au hayo ni juu ya vijitabu mamia vilivyopata kuandikwa, au juu ya biblia ilivyo sasa ipi yenye vijitabu 66 au 72 ? Upeo wa maelezo haya hautafikia kujibu swali hilo.

Dhana kinzanifu nyingine akutanayo msomaji wa Maandiko Matakatifu na vitabu vya elimu dunia ni juu ya kuumbwa kwa vitu vyote na mageuko (evolution). Hizo ni kama imani mbili zisizoyakinishika. Mwenye imani katika vyote kuumbwa naye hawezi kufafanua kwa yakini, pia mwamini juu ya mageuko hawezi kuyahakikisha kwa majaribio ya kisayansi katika maabara kimbilio la Mwanasayansi. Bali ichunguzwapo zaidi huenda mwandishi na mwanasayansi huenda wakawa wanazungumzia jambo linalofanana. Dhana ya mageuko huhusika vipindi virefu vya miaka mingi kupita kufikia hatua hadi hatua. Dhana ya uumbaji hutaja siku sita za vyote kufanyika. Neno ‘siku’ katika lugha iliyotumika enzi za uandishi wa kijitabu cha Mwanzo lina maana pia ya ‘kipindi kirefu cha miaka mingi.’ Hufikirika ya kwamba, siku hizo sita huenda hazikuwa kama siku zilivyo leo zifuatazo kuonekana na kuchwa kwa jua. Kama hivyo ndivyo, haieleweki siku tatu za mwanzo zilikuwaje, maana jua halikuwa limeumbwa hadi siku ya nne (Mwa 1:14-19). Pia labda siku ilivyo kwa mwanadamu huenda ikawa sivyo ilivo kwa Muumbaji wa vyote, katika Maandiko Matakatifu miaka elfu moja hufananishwa na siku moja kwa Mungu (Zab. 90:4).

Kwa kifupi na uchache wa maelezo, Waamini wa Neno la Mungu duniani leo hutumia Biblia katika ‘sura’ kuu tatu; wapo walimwengu wa leo wasioamini ya kwamba Masiha ameshazaliwa, hao Biblia kwao ni Agano la Kale tu. Waaminio kuwa Masiha au Kristu alizaliwa, kafa na kufufuka wamegawanyika makundi makuu mawili; wapo ambao Biblia yao ni yenye vijitabu 66 na wengine 72.

Historia ya sasa bado ina kumbukumbu changa juu ya mjadala ni vijitabu vipi ni vitakatifu. Martin Luther, mwanzilishi wa upinzani kidini aliwahi kususia vijitabu saba kutoka katika Agano Jipya. Alisusia kijitabu cha Waebrania, Yakobo na Waraka wa pili wa Petro. Vinginevyo alivyosusia ni pamoja na Nyaraka mbili za Yohana (2 Yoh. Na 3 Yoh.). Yuda na Ufunuo. Baada ya upinzani huo ulikwisha na Agano Jipya likawa na idadi ya vijitabu ileile kwa makundi hayo makuu mawili ya Wakristo.

Pamoja na yote yaliyoelezwa katika sura hii, lililo la muhimu ni kukiri Maandiko Matakatifu ni kumbukumbu za matukio na maelekezo maalumu ya Muumba kwa Viumbe wake. Mwandishi wake Mkuu ni Mungu alieongoza wanadamu kushika kalamu na kuyaandika yote katika lugha ya kuweza kueleweka na wanadamu.

Soma kitabu kamili hapa (eng) Mungu hutaka nini
- Alphonse Shija Mahuyemba

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Uchawi:Epistemolojia, elimu, kisomo, ushirikina na imani za uchawi katika mauaji ya vikongwe usukumani.
Ni nini kifanyike kumwelimisha na kumzuia kulipiza kisasi, kwa mauaji mzazi anayeamini ya kuwa mtoto wake kauawa kichawi na marehemu alimtaja mchawi wake akiwa kufani!
Je itasaidia nini kuchambua epistemolojia, imani na masimulizi ya usukumani? kisomo na elimu ya kisasa vina mchango gani?
Mauaji kwa imani za kichawi hayakuanzia na wala hayako usukumani tu. Historia ina masimulizi ya Ujerumani.. Na Alphonse S. Mahuyemba
Nakala kamili Hapa

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Hata shetani hutumia biblia na vitabu vitakatifu katika vita yake; tuwe makini
Kuyajua au kuyazoea matumizi ya Biblia huja kwa kuisoma, pia kwa kujuzwa /kufunzwa na waifahamuo. Kwa angalizo tu, ikumbukwe ya kuwa katika vitu vya kiroho silaha yetu ya kuitumia na adui yetu ni hiyo hiyo huweza kuitumia: Katika kumjaribu Yesu, Ibilisi alimwambia “imeandikwa .............. Mat 4:6, Luk 4:10 (atawaamuru malaika wake wakulinde) – baada ya kumtaka Yesu ajitupe chini!
Katika jaribu la Yesu kuamuru mawe yawe mkate; Yesu alimjibu Ibilisi: Mat 4:4, Luk 4:4 (Mtu haishi kwa mkate tu). Baada ya semina hii, washiriki tuepuke laana ya BWANA kwa kwenda kuifanya kazi yake kwa bidii; Yer 48:10, tukipambana ipasavyo katika vita vya kiroho kwa upanga/silaha aliyotupa ambayo ni neno lake, Efe 6:17. Nakala kamili Hapa

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Baada ya dhambi mdhambi akate tamaa ?
Dhambi ni kosa linalovunja amri ya mungu. Mdhambi huweza kuvunja mojawapo ya amri za Mungu kwa mawazo,matendo,mazungumzo au kwa kutokutimiza wajibu. Baada ya dhambi kutendeka kinachohitajika ni mdhambi kutubu. Kwa vile ni Mungu ambaye hutendewa dhambi, msamaha wa dhambi hutolewa na Mungu peke yake. Msamaha wa dhambi hutolewa na Mungu kwa mdhambi aliyetubu kwa dhati kabisa. Kwa vile yeye Mungu huona yaliyo sirini mwa mwanadamu ni toba ya kwelikweli huhitajika ili maondoleo ya dhambi yafanyike.

Ishara ya nje iliyo wazi ya mdhambi ni ile hatua aichukuayo kuonesha toba. Ishara hiyo ya wazi ionekanayo na watu au mtu ikiwa toba ya dhati, kufuatwa na ishara ya ndani sirini ya maondoleo ya dhambi. Mdhambi akinesha kwa nje kutubu bila toba, moyoni mwake, hapati msamaha wa dhambi kutoka kwa aonaye yaliyo sirini. Katika kutekeleza yaliyo wazi ya maondoleo ya dhambi Yesu Kristo, Mungu Mwana, aliwaachia wafuasi wake mamlaka ya kutamka maondoleo ya dhambi (Yoh. 20:21-23).

Neno la kuasa hapa, ni kwamba Yesu alipowaagiza akiwaambia ’mkiwaondolea watu dhambi zao, wameondolewa……’ haina maana ya kwamba wajibu wa mdhambi kutubu kwa dhati uliondolewa. Mdhambi kama hana toba ya dhati moyoni maneno ya ‘muondoa dhambi’ wa ishara ya nje hayana maana.

Maandiko Matakatifu yanayo historia ya dhambi za mdhambi kuondolewa bila toba ya dhati ya mdhambi. Msamaha wa aina hiyo Mungu huutoa kwa makusudio yake maalumu. Msamaha wa bila hiyari ya mdhambi unajidhihirisha kwa yaliyompata Saulo ambaye baadae aliitwa Paulo (1Tim.1:13).

Mungu akishatoa msamaha wa dhambi kwa mdhambi aliyekiri kosa lake Mungu husamehe kabisa. Wanadamu mashuhuri waliowahi kuwa na dosari za kidhambi katika Biblia ni kama vile kina Musa, Daudi na Paulo.

Nabii Musa aliwahi kuvunja amri ya Mungu inayokataza kuua (Mwa. ). Musa alikiri kosa lake akasameheka. Baada ya Musa kusamehewa aliaminika katika maadili hadi kunurulishwa Ya Ufalme wa mbingu na kuyaandika. Musa angalikua mdhambi asiyekiri makosa yake kwa dhati hangalimtumia kama mshika kalamu aliyeandika vijitabu vitano vya kwanza katika Biblia.

Mfalme Daudi alikua ni mwanadamu mwadilifu tangu enzi za ujana wake. Daudi katika kipindi cha ufalme wake alitenda dhambi kwa kitendo cha uzinzi (2 Sam.11:2-) na baadaye kwa hila kusababisha kifo cha mtu asiyekua na hatia (2 Sam.11:14-17). Mfalme Daudi alikiri kosa lake (2 Sam.12:13, 12:16,17. Zab.139:1-18) kwa dhati na kwa kusameheka kabisa hadi kuwa mfano bora wa utakaso katika Biblia.

Mtume Paulo alianzia katika kulinyanyasa kanisa (Mdo.8:3, 9:1,2) hadi kuongoka (Mdo.9:3-19, 22:6-16, 26:12-18) na kuwa Mtume wa Kristo Paulo aliyeitwa Saulo hapo awali alisamehewa na kuongolewa bila hiyari yake.

Paulo alisamehewa bila kuomba msamaha.

Pana msemo kwamba “bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi”. Pamoja na ukweli kuwa baadhi ya misamaha ya dhambi toka kwa Mungu huja kwa neema tu, mdhambi anaowajibu wa kuomba msamaha wa dhambi kwa toba timilifu. Kutenda dhambi na kukata tamaa juu ya msamaha wake hakuna maana. Dhambi hata ikiwa ya uzito au ukubwa wowote Mungu mpendelevu huisamehe. Dhambi yoyote hata ikitisha sana iombee msamaha. Husameheka. Kwa Mungu hakuna lisilowezekana.
- Alphonse Shija MAHUYEMBA

Soma zaidi hapa (kitabu) Vitabu vya kiimani.

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Kuabudu msalaba ni kosa ?
Neno kuabudu lifafanuliwapo kidini ni kuheshimu, kuogopa, kumnyenyekea au kutumikia. Kwa maana hizo zote; anayestahili kuabudiwa ni Mungu YEHOVA. Kwa wivu na mapenzi yake haruhusu kinginecho kuabudiwa. Pamoja na hayo, matumizi mengineyo ya neno kuabudu yana maana ya kuhusudu au kupenda kupindukia. Kwa maana hiyo nyingine, mtu au kitu kinginecho chaweza kuabudiwa. Katika kuabudu msalaba ichukuliwe maana ipi ?

Maelezo ya makatazo ya kuabudu sanamu yanapatikana wa Kikristo kitabu cha Kutoka 20:4-5. Maelekezo katika aya hii ni kutokutengeneza sanamu na kuziabudu. Haiishii kukataza tu bali adhabu ya mkosaji inatajwa katika kijitabu cha kumbukumbu la Torati 27:15. Laana kutoka kwa Mungu inamwandama ajitengenezeaye sanamu kutokana na mawe, miti au chuma na kuiabudu. Baadhi ya askari wa Yuda walimchukiza mungu kwa kuvaa visanamu vya miungu wakaangamizwa vitani (2 Mak. 12:39-42).

Ukweli ulio wazi ni kwamba msalaba sio sanamu, sanamu maana yake ni kitu au kiumbe kilichotengenezwa kwa kuchonga au kufinyanga kuiga umbo la viumbe vilivyoumbwa na Mungu kama vile binadamu au hayawani. Kitu kinginecho kitengenezwacho kufuatia uvumbuzi wa kifundi stadi wa mafundi waliotangulia hakiwi sanamu ya kilichotangulia kuundwa. Huo ni ufundi ambao watu hupokezana kwa sababu hii, msalaba uliotengenezwa na ukatumiwa kumpigilia Kristo juu yake ni matokeo ya kiufundi tu siyo uumbaji. Na misalaba itengenezwayo kwa kifaa cho chote leo ni misalaba itengenezwayo kufuatia ufundi stadi wa awali. Pamoja na ukweli huo ya kwamba msalaba si sanamu bali kazi halisi ya kiufundi isiyoiga umbo wala kiumbe uheshimike kwa kiwango cha kuabudiwa au kuhusudiwa tu.

Yesu Kristo sawa na binadamu wengine wazaliwao, alichukua umbo la binadamu aliyeumbwa na Mungu. Sanamu ya Yesu msalabani ni sanamu ya kuiga kilichoumbwa na Mungu. Kwa hali hiyo ni uangalifu mkubwa sana unahitajika katika kuheshimu msalaba ukiwa na sanamu ya Yesu. Sanamu yo yote iwe ya Yesu au ya ‘Mungu wa kufikirika’ (Hakuna aliyemwona Mungu). Hairuhusiwi kuabudiwa. Msalaba ambao ni kifaa kilichotumika kuhitimisha ukombozi wa wanadamu hustahili nafasi ya pekee katika kumbukumbu akilini mwa wakombolewa. Upekee wa nafasi ya msalaba katika kumbukumbu akilini sharti utenganishwe na hicho kinachomstahili Muumba. Sanamu ya yesu msalabani ikumbushie tu tukio hilo maalumu bali usitumike katika kuabudu ukiabudiwa wenyewe.

Yaelekea makatazo ya utengenezaji wa sanamu hayana maana na sanamu za kiufundi kwa kupamba pahala pa kuishi zinakatazwa. Na pengine hata mungu hakuzikataza ikiwa zitatengenezwa kwa matumizi mengine yasiyo ya kuabudu. Vinginevyo mtu angechunguza Maandiko Matakatifu kijuujuu angeona Mungu mwenye kigeugeu. Maana hapo juu pametajwa kukataza utengenezwaji wa sanamu, mara mwenye kukataza hivyo aamua atengenezwe nyoka wa shaba. Nyoka huyo wa shaba (Hes. 21:9) amefananishwa na kuinuliwa kwa Yesu msalabani katika injili ya Yohana (Yoh. 3:14).

Maagizo mengi ya Mungu huhitaji jambo moja tu, utii. Ni kwa kukosa utii tu dhambi nyingi zimetendeka. Alipoagiza nyoka wa shaba atundikwe juu alitaka watu kutii ya kwamba aliahidi uponyaji kwa kila aliyeumwa na nyoka kwa kuinua macho juu na kumtazama nyoka wa shaba. Mwenye kumtazama nyoka wa shaba aliokoa maisha yake, hakupona kwa ajili ya huyo nyoka aliyeonekana bali kwa ajili ya yeye aliyeahidi uponyaji (Hek. 16:7). Nyoka huyo wa shaba aligeuka kuwa chukizo kwa bwana walipoanza kumuabudu. Maandiko Matakatifu yasema mfalme Hezekia alimfurahisha Mungu alipomvunjavunja yule nyoka wa shaba baada ya kuwa watu walianza kumwabudu (2 Fal. 18:4).

Ikilazimika kukufananisha kuinuliwa kwa Kristo msalabani na kuinuliwa kwa nyoka wa shaba jangwani ilazimike pia kuamini kwa utii kwamba ni juu ya huo msalaba ambapo ukombozi wa watu ulitundikwa. Ikumbukwe ya kuwa Mwabudiwa alitundikwa hapo msalabani bali sanamu yake juu ya huo msalaba ni kitu kilichokatazwa kutengenezwa na kuabudiwa. Bali kama ilivyoelezwa hapo juu huenda ikawa utengenezwaji wa hiyo sanamu kwa matumizi mengine yasiyo ya kuiabudu hayana ubaya kama ilivyojitokeza kwa nyoka wa shaba.

Swali linalobakia ni hili lifuatalo, Katika ufundishaji wa elimu dunia wenye kufundishwa huweza kuonyeshwa vitu halisi wafundishwayo habari zake. Vitu hivyo itokeapo kuwa havipatikani sehemu ya mafunzo, sanamu na picha zake hutumika katika kufundishia. Je, sanamu na picha za yahusuyo Ufalme wa mbinguni hufaa katika kufundishia ?

Kilichokatazwa
katika kutoka 20:4,5 ni kuabudu kwa sanamu na kitu kinginecho isipokuwa YEHOVA (Kut. 20:3). Kwa mfano, hairuhusiwi kumwabudu mwanadamu, mnyama wala mmea kwa kile hali iwayo; halisi au sanamu. Kwa hiyo kila inapobidi kufundisha mambo ya Ufalme wa mbinguni kwa kuandika kwa sanamu au picha, ili kurahisisha ufundishaji, ihakikishwe ya kuwa walengwa wametanabahishwa kutokuviabudu. Swali hili ni muhimu kuzingatiwa katika kuwafundisha ya Ufalme wa mbingu ‘watoto’ (utoto udogo hapa usichukuliwe kwa namna ya umri tu bali ni pamojana wengine wote ambao ni wachanga katika Maandiko Matakatifu). Wa kuabudiwa ni Mungu Muumbaji wa vyote. Bwana haruhusu, ni dhambi kuabudu sanamu au cho chote kilicho duniani angani na mbinguni (Kut. 20:3-5).
Imeandikwa na Alfonsi Shija MAHUYEMBA
Inapatikana katika kitabu Mungu hutaka nini

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Adhabu au maonyo katika kubadili tabia ya mtu/mtoto
Anaandika Ntanguligwa Constantine.
Tafadhali share unaweza okoa maisha na future ya mtoto mmoja wapo Tanzania.
Mungu alipotuumba alitupa fursa ya kipekee hata kwa mapungufu na tofauti tulizonazo kama binadamu. Kwenye mafundisho ya awali ya dini tulifundishwa angalau kuwa Mungu alituumba tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake juu mbinguni.
Kwenye biblia Muhubiri anatuambia kwenye ile sura ya kwanza:
1 Maneno ya Mhubiri
2 Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili.
3 Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?
4 Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima.
5 Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake.
6 Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.
7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena.
8 Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia.
9 Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua.
10 Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi.
11 Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.
12 Mimi, Mhubiri, nalikuwa Mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.
13 Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu, na kuyavumbua kwa hekima; ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.
14 Nimeziona kazi zote zifanywazo chini ya jua; na, tazama, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.
15 Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, Wala yasiyokuwapo hayahesabiki.
16 Nikatafakari nikisema, Nimejipatia hekima nyingi kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; naam, moyo wangu umeona kwa wingi hekima na maarifa.
17 Nikatia moyo wangu ili kuijua hekima, na kujua wazimu na upumbavu; nikatambua ya kwamba hayo yote nayo ni kujilisha upepo.

Katika dunia hii tumeumbwa binadamu na tofauti nyingi sana. Kiuwezo, kifikra, kiakili, kikabila n.k. Ni wazi kwamba sisi ni bora kuliko baadhi na dhaifu kuliko baadhi pia(we are stronger than some and weaker than some). Siku zote tukumbuke tunadhumuni katika maisha yetu katika dunia hii. Kunasababu kwanini tupo.(In each way we must always remember we all have a purpose in the world) hata tuwe dhaifu kiasi gani.

Nataka kusema nini?
Watoto wadogo wapo katika stage ya muhimu sana kwenye maisha yao(walau ninaowazungumzia hapa leo ni wale mpaka miaka 13, ingawa inaweza kuapply na zaidi inapofaa). Angalau kwa mda mfupi niliosoma saikolojia na magonjwa yake ni wazi kwamba stage hii ndiyo inayo determine their future. Nimewiwa kusema haya kwa kuona utofauti uliopo baina ya watoto na familia mbalimbali. Ni wazi kuwa uwezo wao wa darasani unaweza kutofautiana sana, tabia vivyo hivyo na interests(vitu wanavyovipenda) pia.
Je ni dhambi au kosa la nani mtoto kutokuwa na akili za kukokotoa hesabu au kushika nafasi za chini darasani?
Kila kitu ni mpango wa Mungu hakuna dhambi wala makosa rejea (Yeremia 1:5) “kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni. Tofauti hizi huanza tangu mimba inatungwa. From our embryological perspective Mwili na Akili ya binadamu inaweza kubadilika kwa kubadili position ya gene(kinasaba) moja tu(a very tiny organic factor not even visible to the eyes) kwenye uumbaji uanzao tumboni mwa mama na ikasababisha kutokea mtu tofauti kabisa. Ndiyo maana mama mjamzito kwa mfano hashauriwi na ni hatari zaidi kutumia kemikali katika angalau miezi mi3 ya mwanzo ama wiki ya 1-12(1st trimester) sababu hata moshi tu ule wa sigara unaweza badili mtu atakayezaliwa kabisa(teratogens). Nimesoma na kuwafundisha tangu zamani rafiki zangu nikiwa shule. Nimekutana na watu wenye uwezo tofauti tofauti. Waliodhaifu na walio imara pia. Mara zote nimekuwa ninawaelewa na kila mtu natafuta namna nzuri ya kumsaidia nashukuru Mungu wapo wanaonishukuru hata leo kwa walipofika. Zaidi sana mimi si kwamba nilikuwa na akili sana ama bora kuliko wote lakini nilikuwa na bahati tu na baraka za Mungu. (And most of all, i am not the best i was just lucky and blessed.)

Kipindi hiki cha Saikolojia yao watoto. Ni vema kutambua vema udhaifu wao na uwezo wao. Kujaribu kuimarisha zaidi uwezo wao na kutafuta namna nzuri ya kusahihisha mapungufu yao.
Mtaalamu wa sayansi Einsten alisema: If u teach a cat all it life knowing it can fly, it will always live its life knowing it is stupid" yani nyau ukimtrain ajue anaweza kupaa, maisha yake yote atajiona mjinga sababu atashindwa kufanya kitu akichoambiwa anatakiwa aweze ambacho kiuhalisia hakiwezekani. Vivyi hivyo. Kuna kitu nimeobserve tangu nikikua. Mfano Fikra kuwa lazima usome sayansi. Lazima uwe mwanasayansi. Lazima ujue hesabu. Si kweli hata kidogo ndiyo maana muhubiri anasema mambo yote ni ubatili mtupu. Misemo kama hii: Hii hata mjinga anaweza. Statement kuwa you are stupid. Ni hatari sana na za kuvunja moyo kwa mtoto.(These are very dangerous heartbreaking statements to children atleast of that young age). Maisha yao yote wanakuwa wanajua wao ni wajinga tu. Hamna wanachokiweza.

Nitatoa mfano mmoja. Kwenye afya ya akili kuna watu wanapata ugonjwa unaitwa depression. Akili ya binadamu ni kitu cha ajabu sana. Unaweza kukifanya kiamini unavyotaka wewe na ukashangaa mwili mzima utajibadilisha kulingana n akili inachofikiri.
Depression angalau kwaufupi ni hali ambayo mtu anajiona hana uwezo wa kufanya chochote. Kiasi hata ukimwambia mtu simama ufunge pazia atakwambia hawezi si kwasababu hawezi kweli ama kiburi bali ni kwasababu akili yake inafikiri hivyo na pale kweli mwili wake unashindwa kabisa.
Lakini nitagusia moja ya njia tunayoweza kumsaidia mgonjwa wa aina hii. Ukimwambia basi kama huwezi kufunga pazia angalau simama basi. Kile kitando cha kusimama tu atapata kitu tunaita "zawadi kwenye ubongo"(kuna reward system kwenye brain) na atajiona "alaaa"! kumbe naweza. Kutokea hapo taratibu atapata mabadiliko ya mfumo wa kiakili na hatimaye kusema sasa najaribu na kufunga pazia hatimaye anapona kabisa.
Pamoja na magonjwa mengine mengi ya akili(psychopathologies) kama obsessive compulsive disorders, dellussion na Schizophrenia(ambayo huweza jijenga taratibu hasa mtu akipitia mazingira ya msongo wa mawazo, wakikosa upendo) nk.
Ndicho watoto wanachohitaji, upendo na support ya walezi/wazazi. Kumuita mtoto mjinga hamjengei chochote zaidi ya kumfanya ajione hivyo(manipulation of human brain). Saikolojia inaweza kukufanya hapo ulipo mtu ujione kama huna mikono na kweli ukajiona na kujihisi hivyo kabisa, akili ikipewa mazingira sahihi huweza kubadilishwa.(The brain can be manipulated any time and to anyone to work anyhow given specific conditions). Hii inaendana sambamba kabisa kuwachukulia tofauti(ukiwa na watoto wadogo zaidi ya mmoja) sababu ya uwezo wao na mapungufu yao kwamba ikaonekana mmoja anastahili upendo na kujiwa zaidi kuliko mwingine. Ina matokeo mabaya mwishowe. Wanakuwa na woga na kutokujiamini (Its as a bad implication in their future, mentality and growth. They grow with fear, with depression, with no confidence.)
Ndiyo maana wanasaikolojia pia wanatuambia tofauti ya punishment(adhabu) na reinforcement(kiimarishi tabia). Ingawa na zenyewe zimegawanyika kwenye chanya(positive) na negative(hasi) ila kwa ufupi
Punishment hutumika kurestrict/kukomesha tabia flani(inaweza kuwa inayoumiza physically kama fimbo au isiyoumiza kama kutokutoka nyumbani kwenda kucheza)na Reinforcement hutumika kuimarisha tabia flani. Mfano mtoto akiwa ni dhaifu darasani ni dhahiri kuwa tutaangalia chanzo.
Apart from uwezo wake asilia(ambao hatuwezi sana kuufanyia kitu chochote kama ni asili au pengine ni ugonjwa unaoitwa ATTENTION DEFICIT HYPERACTIVE DISORDER wenye dawa zake kabisa ni ugonjwa wa watoto kushindwa kuconcentrate/ kuwa makini ambao ufahamu wake ni ndogo sana kwenye jamii yetu ingawa una dawa zake kabisa)
Lakini kuna kutokuwa msikivu darasani si kwasababu ya ugonjwa tuseme kwasababu ya kucheza akifika nyumbani hazingatii homework/kazi za shule za kufanya nyumbani anazopewa.
Hapa tuna nafasi ya kufanya punishment kwamba hamna kwenda kucheza na mara nyingine hapa ndo unakuta fimbo imetumika mfano hasa asipokuwa msikivu. Hii taratibu itasupress hii tabia ya kutokuwa msikivu.

Lakini lazima tu reinforce tabia hii kwa kumpatia zawadi atakapoonesha mabadiliko chanya/kupanda/kuimprove kwenye somo lolote lile lets say ameimprove historia kutoka 30 mpk 85 hata kama hesabu amefeli bado mfano amepata 20.
Na hapa hapa ndipo tuna nafasi ya kutumia reinforcement ya kuimprove hesabu pia kwa kumuencourage na kumwambia mfano next time ukipanda na hesabu kutoka 20 kwenda juu zaidi nakuongezea zawadi.
Taratibu akirudi nyumbani atakuwa anakumbuka anahitaji kufanya bidii( he/she has to work harder) na atapunguza kucheza na kufanya homework kwanza sababu kisaikolojia ameshatengeneza connection/uhusiano waa kufanya homework, kuimprove/kupanda darasani na kupewa zawadi hata kama atashindwa kufanya vizuri hesabu lakini ataendelea kufanya juhudi na utaendelea kumtia moyo hivyo hvyo.

Hatari iliyopo ukimuita mtoto STUPID(MJINGA), huna akili, na UKAMTENGA!? Ina reinforce failure(kuimarisha kufeli kwake). Inaimarisha mentality kuwa kumbe sina akili. So kwa vile ni mtoto hana uwezo wa kusema sasa inabidi nibadilike hata kama anajua kuwa kuitwa mjinga si jambo zuri(kwamba sasa neno hili lifanye kazi kama punishment). So atakuwa hivyo hivyo ikiendelea kujireinforce zaidi na zaidi.
Mwishowe anakuwa hajiamini kabisa kuwa anaweza kufanya lolote na graph kushuka zaidi na zaidi yani kukosa ile ari ya kupambana, anaona siwezi kufanya kitu na ndiyo basi tena. Kwenda shule sasa ni kama utaratibu tu ambao ameukuta. Ni kwa ufupi sana nimeelezea hilo. Siku zote kuna hatari kubwa kama hizi mbili zisipokuwa balanced yani reinforcement na punishment.
Mimi huwa napenda kusema na kuwambia watu hasa katika sehemu mbalimbali nimekuwa naongoza na kuishi, kuwa siku zote kuna njia ya amani zaidi kutatua matatizo.(there is always a better and peaceful solution to solve any problem and true we always solved the problems in a peaceful way.) Mwanzo 9:12-16 "Anamwambia mimi sitaangamiza tena dunia kwa maji". Mungu aliahidi hataiangamiza tena dunia kwa maji na kutafuta njia nzuri zaidi kuokoa dhambi za wanadamu hata kumleta mwanae wa pekee badala ya kuangamiza dunia nzima. Ni jambo tunaloweza kujifunza kama wanadamu. Despite hasira na frustration zozote tulizonazo wakati wowote, tunaweza kupata amani ya rohoni (we can always eventually find peace) kama mfano huo huo wa gharika kuu! Lord bless us all.
Regards,
Ntanguligwa Constantine(Mwanafunzi wa udaktari chuo kikuu cha Afya na Sayansi Muhimbili)
Ukipata mda tembelea blog yangu kujifunza zaidi hapa: Adhabu
-Ntanguligwa Constantine
Makala nyingine kutoka kwa mwandishi huyu:
Maumivu ya kichwa
Unywaji wa maji

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Taarifa zilizo katika mtandao huu hazilengi kuwa mbadala wa taarifa rasmi kutoka katika vyombo vyenye mamlaka kama, daktari au mtoa huduma ya afya. Au sekta yoyote rasmi. Taarifa na habari hizi ni kwa ajili ya ujuzi tu.