makala sahili

LoGo

Makala za kiupembuzi zilizoandikwa na waandishi makini. Jiandae kupata madini ambayo yatabadilisha au kukufikirisha upya kabisa. Na kama iwapo utapenda kuwa mmoja wa waandishi hawa usisite.

GO_HOME

Makala Zilizochapishwa

Naam zilizopata kuandikwa; Kufungua bofya 'soma zaidi' iliyo kushoto

BPA: Kemikali katika plastiki na risiti za malipo
Bisphenyl A ama BPA ni kemikali inayotumika kuongeza ugumu wa plastiki na kutokeza aina ya plastiki ngumu zijulikanazo kama polycarbonate plastics. Plasiki hizi huwa na nambari kwenye pembetatu katika kitako chake.
Kemikali hii hutumiwa sana pia katika karatasi za risiti na kutokeza karatasi zinazoweza kuandikika kwa joto la kadiri thermal papers. Hii inajumuisha karatasi nyingi za risiti ikiwamo za atm, efd, risiti (luku, mwendokasi) na nyinginezo
Matumizi yake hayakuishia hapo bali hupatikana katika; chupa ngumu za plastiki, makopo ya chuma ya kusindika vyakula (kama tabaka jembamba kwa ndani)

Inavyokupata
Kemikali hii huingia mwilini kupitia njia ya mdomo au ngozi.
Chakula kilichowekwa katika vyombo vyenye kemikali hii hufyonza kiasi cha kutosha na kumuingia mlaji wa chakula hicho. Lakini pia kugusa au kuviringa/kufinyanga risiti mikononi imetajwa kuwa njia inayopeleka BPA moja kwa moja mwilini, kupitia ngozi. Wote walaji na wahusika wanaogawa risiti kwa muda mrefu wametajwa kukutwa na kiwango kikubwa cha BPA katika miili yao.

Walio hatarini
Wanaotumia vifaa ama vyombo vyenye kemikali hiyo
Askari wa usalama barabarani
Wahudumu madukani
Wahudumu tiketi
wajawazito
watoto

Madhara
Kwa kawaida ni kiwango kidogo sana ambacho mtu anaweza kukumbana nacho. Si kemikali ya hatari sana kwa walaji.
Pamoja na kuwa baadhi ya tafiti zimekuwa zikipinga uhusiano wa moja kwa moja na magonjwa au matatizo kiafya, kutokana na kutokuwepo kwa vielelezo vya kutosha vya uhusiano scausality. Lakini uwepo wa kiwango kikubwa cha kemikali hii imekuwa ikihusishwa na matatizo kama, uzazi, uzito, matatizo ya rovu, kisukari, matatizo ya kinga ya mwili (kupambana na tishu za mwili).
Hii inatokana na sifa ya kemikali hii kufanana na homoni ya estrojeni na hivyo kuvuruga vipokezi vya asili vya homoni hiyo. Kutokana na sababu za kimaumbile wanawake huathiriwa zaidi (wana vipokezi vingi zaidi)
Watu walio katika hatari zaidi ni watoto na wajawazito wakifuatiwa na wanawake na wazee. Na yote inatokana na wao kuwa tayari na vitu vingine vinavyoathiri mfumo wa kawaida wa homoni.
Kwa kawaida mwili huwa na uwezo wa kuiondoa kemikali hii kwa michakato katika ini hasa iliyopita kwa njia ya chakula. Ugumu upo hasa kwa njia ya ngozi au kwa watu wenye mafuta mwilini maana kemikali hii hubaki imeshikamana na mafuta hayo (Kow 2.2).

Kujikinga
Ni vema kuwa na tahadhari zifuatazo. Usitumie chombo chenye bpa kupasha joto, kutunza chakula cha moto. Gusa vifaa hivyo ukiwa na mikono mikavu
Kula chakula bora (Kusaidia utendaji wa mwili kuiondoa kemikali hiyo kwa usalama kabisa glutathione conjugation)
Mtindo bora wa maisha

Soma zaidi hapa (eng) Bisphenyl A.PDF Au hapa WHO BPA Hapa pia NIH report
- Mashauri

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Uchawi:Epistemolojia, elimu, kisomo, ushirikina na imani za uchawi katika mauaji ya vikongwe usukumani.
Ni nini kifanyike kumwelimisha na kumzuia kulipiza kisasi, kwa mauaji mzazi anayeamini ya kuwa mtoto wake kauawa kichawi na marehemu alimtaja mchawi wake akiwa kufani!
Je itasaidia nini kuchambua epistemolojia, imani na masimulizi ya usukumani? kisomo na elimu ya kisasa vina mchango gani?
Mauaji kwa imani za kichawi hayakuanzia na wala hayako usukumani tu. Historia ina masimulizi ya Ujerumani.. Nakala kamili Hapa

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Maumivu matamu
Naam kila mmoja amewahi kusikia ama kupata maumivu kwa namna moja au nyingine. Ile hali ya uchungu ama utungu inayojitokeza kutokana na hali au jambo fulani baya. Baya. Nasisitiza baya kwa sababu maalumu. Maumivu yoyote ni matokeo ya wazo hili.
Kwa tafsiri yake maumivu ni hisia chungu/mbaya inayotokana na kichocheo sumbufu. Kichocheo hiki chaweza kuwa cha kikemikali, cha kimwili au kisaikolojia. Imezoeleka zaidi kwa maumivu ya kimwili kutokeza maumivu ya kisaikolojia baadae, lakini kinyume chake inaweza kutokea pia. Yaani maumivu ya kisaikolojia kutokeza maumivu ya kimwili.

Kwanza tujiulize, kwa nini tuumie? au kuna faida gani ya kuhisi maumivu?
Maumivu hutoa ishara ya wazi ya hatari kwamba kuna kitu kibaya kimetokea au kinatokea. Hii ipo kwa sababu za kiusalama na kimageuzi. Maumivu huokoa uhai maana ni lazima utafanya juu chini kuondoka katika eneo linalokuletea maumivu. Au kutokana na maumivu itakulazimu kupumzisha kiungo husika (kama ni mwilini) ili kutoa muda wa kujirekebisha baada ya ajali. Kumbuka mahala penye maumivu pana kemikali zile hasa zinazohitajika kukusanya nishati na vitu vyote vinavyosaidia mchakato wa uponaji.
Kila mara tunapohisi maumivu tambua kwamba hiyo ni ishara tu ya kuwa mabo hayaendi sawa mahala fulani. Mara nyingi hisia hii hutokea bila utashi wetu. Watoto wadogo kutokana na utashi wao mdogo vitu vingi vyaweza kuwaumiza. Chochote watakachohisi kuwa ni kibaya. Lakini kadiri tunavyokua ndivyo tunazidi kujifunza kwamba baadhi ya vitu si hatari na havituumizi tena!.
Kwa mfano pilipili. Pilipili ina kemikali ijulikanayo kama capscain ambayo ndiyo hukipa sifa kiungo hiki adhimu. Kemikali hii husisimua vipokezi vya joto katika mwili na kutokeza taarifa inayosomeka na ubongo kama 'joto kali', ama 'chakula ni cha moto sana'. Taarifa hii huaminika kabisa kwa mtoto ambaye hudhani kuwa hiyo ni hatari haswaa na hutafsiri kuwa ni maumivu. Akaangua kilio. Lakini mtu mzima anatambua fika kuwa wala hapana joto kali kiasi hicho na hivyo badala ya maumivu, yeye hupatwa na maumivu matamu.
Imethibitika kwamba kupatwa na maumivu ya kiwango cha chini tofauti na uliyotarajia huleta furaha. Na hapa ndipo lilipozaliwa hili wazo la maumivu matamu.
Hivyo basi ili mtu apatwe na maumivu ni lazima ahisi/aamini/ajue kuwa kuna kitu kibaya kimetokea. Bila yeye kupitisha kuwa ni kibaya hatahisi maumivu kamwe. Hili linajionesha wazi katika maumivu ya kisaikolojia. Na hata ukichunguza vizuri, maumivu mengine nayo yana muundo huohuo.

Namna ya kutatua matatizo
Matumizi ya dawa za kutuliza maumivu ndiyo njia inayotumika zaidi kuondoa maumivu. Ni muhimu kutatua chanzo cha maumivu hayo nayo yatapotea menyewe. Hivyo kujua chanzo ni muhimu.
Na kwa maumivu ambayo chanzo chake ni kisaikolojia, kutazama upya hali hiyo kwa kujaribu kujenga picha nzuri ya tukio itasaidia. Kama kuna uwezekano wa kufanya tukio likaonekana si la hatari basi maumivu yatakwisha. Wazo chanya hapa ni muhimu sana.
Kufanya mazoezi au shughuli yeyote inayokupa furaha na kukuondolea mawazo. Mzunguko mzuri wa damu na oksijeni husaidia kuondoa maumivu.
Kupuuzia hali iliyopo pia husaidia sana. Tuchukulie mfano dawa kali aina ya morphine, moja ya kitu inachokifanya ni kumfanya mgonjwa asiyachukulie maumivu aliyonayo kwa uzito wowote na badala yake afanye/afikirie mambo mengine.
Mazoezi ya akili na namna ya kufikiri yatawafaa sana watu hasa wenye maumivu ya kudumu yasiyo elezeka chanzo. - Mashauri

Soma zaidi hapa (eng) Pain; The pleasant truth about it.

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Virusi au kirusi sio kiumbe cha ajabu; Ni taarifa tu
Tangu kugundulika kwake, virusi vimewaacha midomo wazi wanasayansi na wanataaluma kutokana na uajabu wake. Maajabu yake yapo katika kukosa kwake sifa kadhaa ambazo kiumbe hai anapaswa kuwa nazo. Na hata sasa hakuna muafaka yakuwa ni kiumbe hai ama si kiumbe. Tafsiri yake imebaki kuwa ‘Kirusi ni kipande kidogo sana chenye jeni (chembeurithi) iliyozungukwa nap rotini, vipande hivi huambukiza seli na kuzaliana katika seli husika.
Kama inavyofahamika kwamba kwamba jeni ndicho kitu pekee kinachoweza kuhamisha na kutunza taarifa katika viumbe hai. Na muundo wake ni tata sana, sana.. sana. Basi tunaweza kusema kwamba virusi ni vipande vya taarifa kutoka katika seli moja kwenda kwenye nyingine. Au kutoka kwa kiumbe mmoja kwenda kwa kiumbe mwingine.

Taarifa
Ni ujumbe kutoka upande mmoja hadi mwingine. Ujumbe huu huweza kuwa ndio umezalishwa na huyo anayetuma ama yeye anasambaza kile tu alichoambiwa ama kusikia.
Tunasambaza taarifa za hatari kwa haraka zaidi ili wapendwa wetu wachukue tahadhari
Taarifa nyingine huweza kuwa maarufu kiasi kwamba ni kila mtu anajua hivyo na anatenda kulingana na ujumbe husika.
Wakati mwingi tunasambaza taarifa bila kuulizwa nahiyo ni ili kuwalinda tunaowapenda na wanaotuzunguka, tunahisi ni jukumu letu kabisa.
Basi kutokana na hayo tuliyoyaona na tunayoyafanya kiasili kabisa ndivyo seli zetu hufanya vivyo hivyo. Pale seli inapohisi ina taarifa ya muhimu kuwafikishia seli nyingine inaweza kutumia baadhi ya njia zifuatazo;
Kutumia mnunurisho, kwa kuzalisha mawimbi ya umeme au sauti au miali yoyote yenye uwezo huo. Mfano seli za neva.
Kutumia molekyuli ndogo au kemikali rahisi kama sodiamu au kalisiamu. Kwa mfano misuli.
Kuzalisha kemikali tata za protini mafuta au viungo vingine. Kwa mfano estrojeni na thairoksini.
Kutumia jeni zenye taarifa husika. Mfano bakteria wanavyofundishana usugu kwa kupitia plasmidi
Njia ya mwisho haitumiki sana katika mawasiliano ya kawaida. Bali hutumika katika mawasiliano ya muhimu na ya siri. Kama vile kujilinda na hatari inayozikabili seli za jamii husika. Seli za jamii husika zinaweza kuwa katika kiumbe huyohuyo au kwa kiumbe mwingine. Na vipande vya taarifa hizo ndizo huitwa virusi. Nitasema hivyo kwa mifano:

Mafua
Maambukizi ya virusi katika njia ya hewa husababisha kutokwa na mafua mepesi. Kuna namna nyingine za mafua zitokanazo na sababu nyingine lakini tutaongelea haya yatokanayo na virusi.
Mafua haya husambaa kwa kasi wakati wa baridi. Wakati huu ambapo hewa huwa ya baridi na kavu ndipo hasa msimu wake.
Ifahamike kuwa hewa ya baridi sana huumiza njia ya hewa (Ndiyo maana kuna asthma). Hewa kavu vivyo hivyo. Kwa kawaida hewa hupita puani kupatiwa unyevu na joto lifaalo kabla ya kufika kwenye mapafu.
Ni muhimu basi kuwa na maji/unyevu wa kutosha wakati huo ili kuwezesha hayo. Na seli inayopata taarifa hii ama kwa kuianzisha, au kusikia huona ni vyema kuwajulisha wenzake. Na kwa kuwa taarifa hii inapaswa kuwa mahsusi na itapita maeneo mengine mengi basi huwekwa katika mfumo wa siri (code) kisha kusambazwa.
Seli nyingine itakayopokea hutumia na kufanya vivyo hivyo! Na taarifa/mafua/kirusi husambaa kirahisi.

Virusi vinavyohusishwa na kansa/saratani
Kuna swali watu hujiuliza iwapo kansa huambukiza? Je kansa huweza kutoka kwa mgonjwa mwingine kwenda kwa mwingine, jibu ni hapana na ndiyo.
Kansa ni mwitikio wa seli kujilinda na hali ngumu ya kimaisha kama kemikali au miali mikali. (Soma zaidi hapa Saratani.) Virusi hivi hutumika kutoa taarifa kwa seli nyingine ili ziige mfano wa kujizalisha. Sasa itategemea na hizo seli nyingine. Zikihisi hakuna matatizo au mazingira magumu zitapuuzia. Endapo zikihisi kuna ulazima wa kukua(kujiongeza) basi zitafanya hivyo. Kwa mfano Human papiloma virus (HPV). Umri mdogo kuanza kufanya mapenzi na idadi ya wanaume imetajwa kuwa chanzo kwa mwanamke husika. Lakini mwanamke anaweza kupata taarifa/virusi kutoka kwa mwanaume wake na kupata kansa ya uzazi.

Mwisho kama ilivyo kwa taarifa nyingine, basi wapo watu wanaozipokea na kufanyia kazi, wengine hupuuzia. Wengine huamua kuzibadili, taarifa nyingine ni za uongo. Vivyo hivyo na virusi watu wengine hawaugui hata wapatapo virusi. Na si rahisi kurudia tena kufanyia kazi taarifa ambayo tayari unaujua mwisho wake kuwa si hatari na ndiyo maana kuugua mara mbili kirusi wa aina moja sio kawaida sana. Angalau kwa muda mfupi, lakini endapo umepita muda mrefu tangu kupata virusi/taarifa fulani basi kuna uwezekano wa kuugua tena. Kuugua mafua mara mbili katika msimu mmoja si kawaida.
-Mashauri

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Adhabu au maonyo katika kubadili tabia ya mtu/mtoto
Anaandika Ntanguligwa Constantine.
Tafadhali share unaweza okoa maisha na future ya mtoto mmoja wapo Tanzania.
Mungu alipotuumba alitupa fursa ya kipekee hata kwa mapungufu na tofauti tulizonazo kama binadamu. Kwenye mafundisho ya awali ya dini tulifundishwa angalau kuwa Mungu alituumba tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake juu mbinguni.
Kwenye biblia Muhubiri anatuambia kwenye ile sura ya kwanza:
1 Maneno ya Mhubiri
2 Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili.
3 Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?
4 Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima.
5 Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake.
6 Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.
7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena.
8 Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia.
9 Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua.
10 Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi.
11 Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.
12 Mimi, Mhubiri, nalikuwa Mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.
13 Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu, na kuyavumbua kwa hekima; ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.
14 Nimeziona kazi zote zifanywazo chini ya jua; na, tazama, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.
15 Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, Wala yasiyokuwapo hayahesabiki.
16 Nikatafakari nikisema, Nimejipatia hekima nyingi kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; naam, moyo wangu umeona kwa wingi hekima na maarifa.
17 Nikatia moyo wangu ili kuijua hekima, na kujua wazimu na upumbavu; nikatambua ya kwamba hayo yote nayo ni kujilisha upepo.

Katika dunia hii tumeumbwa binadamu na tofauti nyingi sana. Kiuwezo, kifikra, kiakili, kikabila n.k. Ni wazi kwamba sisi ni bora kuliko baadhi na dhaifu kuliko baadhi pia(we are stronger than some and weaker than some). Siku zote tukumbuke tunadhumuni katika maisha yetu katika dunia hii. Kunasababu kwanini tupo.(In each way we must always remember we all have a purpose in the world) hata tuwe dhaifu kiasi gani.

Nataka kusema nini?
Watoto wadogo wapo katika stage ya muhimu sana kwenye maisha yao(walau ninaowazungumzia hapa leo ni wale mpaka miaka 13, ingawa inaweza kuapply na zaidi inapofaa). Angalau kwa mda mfupi niliosoma saikolojia na magonjwa yake ni wazi kwamba stage hii ndiyo inayo determine their future. Nimewiwa kusema haya kwa kuona utofauti uliopo baina ya watoto na familia mbalimbali. Ni wazi kuwa uwezo wao wa darasani unaweza kutofautiana sana, tabia vivyo hivyo na interests(vitu wanavyovipenda) pia.
Je ni dhambi au kosa la nani mtoto kutokuwa na akili za kukokotoa hesabu au kushika nafasi za chini darasani?
Kila kitu ni mpango wa Mungu hakuna dhambi wala makosa rejea (Yeremia 1:5) “kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni. Tofauti hizi huanza tangu mimba inatungwa. From our embryological perspective Mwili na Akili ya binadamu inaweza kubadilika kwa kubadili position ya gene(kinasaba) moja tu(a very tiny organic factor not even visible to the eyes) kwenye uumbaji uanzao tumboni mwa mama na ikasababisha kutokea mtu tofauti kabisa. Ndiyo maana mama mjamzito kwa mfano hashauriwi na ni hatari zaidi kutumia kemikali katika angalau miezi mi3 ya mwanzo ama wiki ya 1-12(1st trimester) sababu hata moshi tu ule wa sigara unaweza badili mtu atakayezaliwa kabisa(teratogens). Nimesoma na kuwafundisha tangu zamani rafiki zangu nikiwa shule. Nimekutana na watu wenye uwezo tofauti tofauti. Waliodhaifu na walio imara pia. Mara zote nimekuwa ninawaelewa na kila mtu natafuta namna nzuri ya kumsaidia nashukuru Mungu wapo wanaonishukuru hata leo kwa walipofika. Zaidi sana mimi si kwamba nilikuwa na akili sana ama bora kuliko wote lakini nilikuwa na bahati tu na baraka za Mungu. (And most of all, i am not the best i was just lucky and blessed.)

Kipindi hiki cha Saikolojia yao watoto. Ni vema kutambua vema udhaifu wao na uwezo wao. Kujaribu kuimarisha zaidi uwezo wao na kutafuta namna nzuri ya kusahihisha mapungufu yao.
Mtaalamu wa sayansi Einsten alisema: If u teach a cat all it life knowing it can fly, it will always live its life knowing it is stupid" yani nyau ukimtrain ajue anaweza kupaa, maisha yake yote atajiona mjinga sababu atashindwa kufanya kitu akichoambiwa anatakiwa aweze ambacho kiuhalisia hakiwezekani. Vivyi hivyo. Kuna kitu nimeobserve tangu nikikua. Mfano Fikra kuwa lazima usome sayansi. Lazima uwe mwanasayansi. Lazima ujue hesabu. Si kweli hata kidogo ndiyo maana muhubiri anasema mambo yote ni ubatili mtupu. Misemo kama hii: Hii hata mjinga anaweza. Statement kuwa you are stupid. Ni hatari sana na za kuvunja moyo kwa mtoto.(These are very dangerous heartbreaking statements to children atleast of that young age). Maisha yao yote wanakuwa wanajua wao ni wajinga tu. Hamna wanachokiweza.

Nitatoa mfano mmoja. Kwenye afya ya akili kuna watu wanapata ugonjwa unaitwa depression. Akili ya binadamu ni kitu cha ajabu sana. Unaweza kukifanya kiamini unavyotaka wewe na ukashangaa mwili mzima utajibadilisha kulingana n akili inachofikiri.
Depression angalau kwaufupi ni hali ambayo mtu anajiona hana uwezo wa kufanya chochote. Kiasi hata ukimwambia mtu simama ufunge pazia atakwambia hawezi si kwasababu hawezi kweli ama kiburi bali ni kwasababu akili yake inafikiri hivyo na pale kweli mwili wake unashindwa kabisa.
Lakini nitagusia moja ya njia tunayoweza kumsaidia mgonjwa wa aina hii. Ukimwambia basi kama huwezi kufunga pazia angalau simama basi. Kile kitando cha kusimama tu atapata kitu tunaita "zawadi kwenye ubongo"(kuna reward system kwenye brain) na atajiona "alaaa"! kumbe naweza. Kutokea hapo taratibu atapata mabadiliko ya mfumo wa kiakili na hatimaye kusema sasa najaribu na kufunga pazia hatimaye anapona kabisa.
Pamoja na magonjwa mengine mengi ya akili(psychopathologies) kama obsessive compulsive disorders, dellussion na Schizophrenia(ambayo huweza jijenga taratibu hasa mtu akipitia mazingira ya msongo wa mawazo, wakikosa upendo) nk.
Ndicho watoto wanachohitaji, upendo na support ya walezi/wazazi. Kumuita mtoto mjinga hamjengei chochote zaidi ya kumfanya ajione hivyo(manipulation of human brain). Saikolojia inaweza kukufanya hapo ulipo mtu ujione kama huna mikono na kweli ukajiona na kujihisi hivyo kabisa, akili ikipewa mazingira sahihi huweza kubadilishwa.(The brain can be manipulated any time and to anyone to work anyhow given specific conditions). Hii inaendana sambamba kabisa kuwachukulia tofauti(ukiwa na watoto wadogo zaidi ya mmoja) sababu ya uwezo wao na mapungufu yao kwamba ikaonekana mmoja anastahili upendo na kujiwa zaidi kuliko mwingine. Ina matokeo mabaya mwishowe. Wanakuwa na woga na kutokujiamini (Its as a bad implication in their future, mentality and growth. They grow with fear, with depression, with no confidence.)
Ndiyo maana wanasaikolojia pia wanatuambia tofauti ya punishment(adhabu) na reinforcement(kiimarishi tabia). Ingawa na zenyewe zimegawanyika kwenye chanya(positive) na negative(hasi) ila kwa ufupi
Punishment hutumika kurestrict/kukomesha tabia flani(inaweza kuwa inayoumiza physically kama fimbo au isiyoumiza kama kutokutoka nyumbani kwenda kucheza)na Reinforcement hutumika kuimarisha tabia flani. Mfano mtoto akiwa ni dhaifu darasani ni dhahiri kuwa tutaangalia chanzo.
Apart from uwezo wake asilia(ambao hatuwezi sana kuufanyia kitu chochote kama ni asili au pengine ni ugonjwa unaoitwa ATTENTION DEFICIT HYPERACTIVE DISORDER wenye dawa zake kabisa ni ugonjwa wa watoto kushindwa kuconcentrate/ kuwa makini ambao ufahamu wake ni ndogo sana kwenye jamii yetu ingawa una dawa zake kabisa)
Lakini kuna kutokuwa msikivu darasani si kwasababu ya ugonjwa tuseme kwasababu ya kucheza akifika nyumbani hazingatii homework/kazi za shule za kufanya nyumbani anazopewa.
Hapa tuna nafasi ya kufanya punishment kwamba hamna kwenda kucheza na mara nyingine hapa ndo unakuta fimbo imetumika mfano hasa asipokuwa msikivu. Hii taratibu itasupress hii tabia ya kutokuwa msikivu.

Lakini lazima tu reinforce tabia hii kwa kumpatia zawadi atakapoonesha mabadiliko chanya/kupanda/kuimprove kwenye somo lolote lile lets say ameimprove historia kutoka 30 mpk 85 hata kama hesabu amefeli bado mfano amepata 20.
Na hapa hapa ndipo tuna nafasi ya kutumia reinforcement ya kuimprove hesabu pia kwa kumuencourage na kumwambia mfano next time ukipanda na hesabu kutoka 20 kwenda juu zaidi nakuongezea zawadi.
Taratibu akirudi nyumbani atakuwa anakumbuka anahitaji kufanya bidii( he/she has to work harder) na atapunguza kucheza na kufanya homework kwanza sababu kisaikolojia ameshatengeneza connection/uhusiano waa kufanya homework, kuimprove/kupanda darasani na kupewa zawadi hata kama atashindwa kufanya vizuri hesabu lakini ataendelea kufanya juhudi na utaendelea kumtia moyo hivyo hvyo.

Hatari iliyopo ukimuita mtoto STUPID(MJINGA), huna akili, na UKAMTENGA!? Ina reinforce failure(kuimarisha kufeli kwake). Inaimarisha mentality kuwa kumbe sina akili. So kwa vile ni mtoto hana uwezo wa kusema sasa inabidi nibadilike hata kama anajua kuwa kuitwa mjinga si jambo zuri(kwamba sasa neno hili lifanye kazi kama punishment). So atakuwa hivyo hivyo ikiendelea kujireinforce zaidi na zaidi.
Mwishowe anakuwa hajiamini kabisa kuwa anaweza kufanya lolote na graph kushuka zaidi na zaidi yani kukosa ile ari ya kupambana, anaona siwezi kufanya kitu na ndiyo basi tena. Kwenda shule sasa ni kama utaratibu tu ambao ameukuta. Ni kwa ufupi sana nimeelezea hilo. Siku zote kuna hatari kubwa kama hizi mbili zisipokuwa balanced yani reinforcement na punishment.
Mimi huwa napenda kusema na kuwambia watu hasa katika sehemu mbalimbali nimekuwa naongoza na kuishi, kuwa siku zote kuna njia ya amani zaidi kutatua matatizo.(there is always a better and peaceful solution to solve any problem and true we always solved the problems in a peaceful way.) Mwanzo 9:12-16 "Anamwambia mimi sitaangamiza tena dunia kwa maji". Mungu aliahidi hataiangamiza tena dunia kwa maji na kutafuta njia nzuri zaidi kuokoa dhambi za wanadamu hata kumleta mwanae wa pekee badala ya kuangamiza dunia nzima. Ni jambo tunaloweza kujifunza kama wanadamu. Despite hasira na frustration zozote tulizonazo wakati wowote, tunaweza kupata amani ya rohoni (we can always eventually find peace) kama mfano huo huo wa gharika kuu! Lord bless us all.
Regards,
Ntanguligwa Constantine(Mwanafunzi wa udaktari chuo kikuu cha Afya na Sayansi Muhimbili)
Ukipata mda tembelea blog yangu kujifunza zaidi hapa: Adhabu
-Ntanguligwa Constantine
Makala nyingine kutoka kwa mwandishi huyu:
Maumivu ya kichwa
Unywaji wa maji

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Kazi za viinilishe mwilini
Vitamini A
Mboga za majani zina kiini-ghafi cha vitamin A (ß-carotene) ambacho wakati wa mumeng’enyo wa chakula hubadilishwa kuwa vitamnini A kamili.
Kazi za Vitamini A:
Vitamini A ni muhimu katika kudumisha afya ya chembechembe-tete za ngozi.
Huimarisha nguvu ya macho kuona; na hasa penye mazingira ya mwanga hafifu.
Huzuia kudumaa katika makuzi; huchangia katika kasi bora ya ukuaji wa viumbe wachanga (watoto).
Huzuia mabakabaka (vibarango) yatokanayo na ukosefu wa vitamin A.
Upungufu/ukosefu wa vitamini A husababisha kudumaa, ukavu wa ngozi, vibarango na upofu katika mwanga hafifu.

Vitamini B1 (thiamine)
Hii ni vitamini muhimu isaidiayo mwili katika kumeng’enya chakula cha wanga (hamilojo).
Ukosefu wa vitamnini B1 husababisha dalili za mapungufu katika utendaji wa neva za fahamu (beriberi).

Vitamini B2 (riboflavin)
Vitamini B2 ina mchango katika mwili kumeng’enya protini (utomwili).
Ukosefu wa vitamini B2 husababisha magonjwa ya ngozi na kufanya vijeraha katika ngozi kutopona upesi.

Vitamini B6 (pyridoxine)
Vitamini B6 ni muhimu katika umeng’enyaji wa viini-tete vya protini (amino acids).
Upungufu wa vitamini B6 husababisha matatizo katika mfumo wa neva za fahamu. Kwa binadamu hali hiyo huambatana na mavune (uchovu), mifadhaiko, kung’aka (nafsini) kusiko na sababu, kukosa usingizi, pia panaweza kuwa na matatizo katika kutembea.

Vitamini B12 (cobolamine)
Vitamini hii huungana na madini ya koboti (cobalt) katika utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu: Upungufu wa vitamin B12 husababisha upungufu wa damu.

Vitamini E (tocopherol)
Vitamini E ni muhimu katika kuimarisha afya ya ngozi, na huboresha mzunguko wa damu mwilini. Vitamini hii pia huboresha na kuimarisha kinga ya mwili na afya ya uzazi.

Vitamini D (calciferol)
Binadamu hujitengenezea vitamnin D chini ya ngozi yake maadam tu awe ameota jua la asubuhi lisilo na joto kali; na awe pia amekula mboga za majani.
Umuhimu wa vitamini D umo katika kuuwezesha mwili kutumia madini ya kalsiumu na fosforasi; hayo ni madini ambayo mwili huyatumia kujitengenezea na kuimarisha mifupa: Vitamini D huongeza kasi ya madini hayo kuchukuliwa kwenda mwilini kutoka kwenye utumbo.
Upungufu wa vitamin D husababisha miguu na mifupa mingine kupinda (matege) kwa watoto wadogo na wanyama wengine ambao wangali wanakua.

Vitamini K
Vitamini K inahusika katika kutengeneza kisababisho cha damu kuganda (prothrombin). Upungufu wa vitamin hii unaweza kuwa na dalili za upungufu wa damu, ongezeko la utokwaji damu na kasi ndogo ya damu kuganda. Mboga za majani ni chanzo kizuri cha vitamini hii.

MADINI
Madini ya Chuma (Fe)
Madini ya chuma (Fe) ni sehemu muhimu ya chembechembe nyekundu za damu: Mwili uwapo na madini ya chuma ya kutosha huimarisha utengenezaji wa damu. Upatikanaji wa madini ya chuma mwilini huimarisha na kuboresha utendaji kazi wa mfumo wa neva za fahamu (taamuli).
Upungufu/ukosefu wa madini ya chuma mwilini husababisha upungufu wa damu. Upungufu huo pia huambatana na dalili za mavune (uchovu wa mwili), uchovu wa misuli, upungufu wa usitahimilivu (stamina); ugumu wa kujifunza kizingativu na mapungufu katika uwezo wa kutatua matatizo (problem solving disabilities).

Madini ya Kalsiumu (Ca)
Madini ya kalsiumu (Ca) huimarisha mifupa na meno. Kalsiumu ikiwa pamoja na fosforasi hudumisha ugumu na uimara wa mifupa na meno. Mwili hujitunzia akiba ya kalsiumu yake kwenye mifupa. Akiba hiyo huweza kutumika kwa uwezesho wa vitamin D pawapo na mahitaji ya ziada mwilini kwa mfano wakati wa kunyonyesha.
Vile vile kazi nyingine ya kalsiumu ni kuwezesha damu kuganda kirahisi. Pia, kalsiumu, ni muhimu katika utendaji kazi wa neva za fahamu na unyumbulifu wa misuli mwilini.

Madini ya Fosforasi (P)
Fosforasi (P) ikiwa na kalsiumu huimarisha mifupa na meno. Mifupa ni kiungo kitunzacho akiba ya fosforasi na kalsiumu mwilini.
Kuwapo kwa vitamin D mwilini huboresha ‘ufyonzaji’ wa kalsiumu na fosforasi kutoka kwenye utumbo na kuingizwa kwenye mfumo wa uimarishaji wa afya ya mifupa na meno. Patokeapo mahitaji ya ziada ya madini hayo; vitamini D huwezesha utoaji wa homoni (parathyroid hormone) ambayo hurahisisha upatikanaji wa kalsiumu na fosforasi kutoka kwenye akiba yake (katika mifupa) mwilini.

Utomwili (Protein)
Kiinilishe cha utomwili (protein) ni malighafi muhimu katika kujenga mwili wa kiumbe hai. Protini iundayo sehemu nyingi za mwili (hasa misuli) hutokana na viinilishe-tete vya aina mbalimbali za tindikali (Amino acids). Kutokana na aina hizo za tindikali hutengenezwa aina mbalimbali za protini ambazo huunda misuli, vitendanishi katika mumeng’enyo (enzymes), homoni, vilainisho na kadhalika.
- Alphonse Shija MAHUYEMBA

Soma zaidi hapa (kitabu) Vitabu sahili

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

Mitishamba katika kudhibiti maradhi/magonjwa na visumbufu
Matumizi ya dawa za mitishamba kutibia binadamu na mifugo yamezoeleka, bali matumizi ya mimea kutibu mimea mingine bado hayajaenea sana. Lakini ni sharti ikumbukwe ya kuwa kila udhibiti wa maradhi na visumbufu unapofanyika kuna kinachouawa: Kwa hiyo ni wazi kwamba sumu katika viwango maalumu hutumika ili kuua kisichohitajika na kuhuisha kinachohitajika. Dhana hii ni wasia mkuu katika kufuata kwa usahihi vipimo vya dawa na sumu zitumikazo katika tiba na kudhibiti wadudu waharibifu.

Dawa na sumu nyingi zitengenezwazo viwandani zina manufaa na madhara yajulikanayo. Kwa upande mwingine; dawa na sumu za kutokana na mitishamba hazijafanyiwa utafiti wa kina hadi sasa. Ukweli huu unaashiria ya kuwa chunguzi mbalimbali zinahitajika katika matayarisho na matumizi ya dawa na sumu za wadudu waharibifu zitokanazo na mitishamba.

Yaelekea kujitokeza ya kwamba dawa na sumu za mitishamba zitaendelea kukubalika katika kilimo kitumiacho teknolojia hai. Dawa na sumu hizo huisha mapema katika mazingira zinamotumiwa. Kinyume chake kemikali za viwandani zitokanazo na kusanidi au kusubu kwa kemikali nyenzie haziishi upesi kwenye mazingira. Kwa kutochakaa na kusambaana upesi kwa kemikali za kusubu (synthetic) uwezo wake wa kuua huendelea na huua baadhi ya vidubini vya kuozesha kwa muda mrefu katika mazingira husika. Sumu za kemikali hizo kwa kudumu kurefu kwenye mazingira, baadaye hutoa mchango wake kwenye uchafuzi wa mazingira.

Pamoja na ukweli ulio hapo juu, dawa na sumu za mitishamba zisikubalike kiholela bila dukuduku! Dawa na sumu hizo hufanya kazi zake kutokana na uwezo wake wa kuua kisichohitajika na kuhuisha kinachotakiwa kiishi. Bila kipimo sahihi hasa katika kuzidisha dawa na sumu za mitishamba zinao uwezo wa kuua kilichokusudiwa na kisichokusudiwa!

Mtayarishaji na mtumiaji wa sumu za kuulia wadudu zitokanazo na mimea sharti awe mwangalifu. Sumu na hata dawa za mitishamba sharti zitunzwe mbali na watoto na wanyama wafugwao. Mtayarishaji na mtumiaji sumu za mitishamba ni lazima ajikinge asidhurike; aujali mwelekeo wa upepo na kutumia mipira ya mikononi (kusetiri viganja na vidole) na baadaye kuvua nguo alizovaa wakati wa kuwa na sumu hizo. Nguo zilizotumika wakati huo zifuliwe kwa maji mengi naye mtumiaji aoge kwa maji na sabuni kabla ya kushika wala kula chochote.

Baada ya kupatiwa ya tahadhari yaliyo kwenye utangulizi huu, sasa inafuata orodha ya baadhi ya mitishamba itumikayo katika kudhibiti maradhi na wadudu waharibifu kwa mazao ya mkulima na mfugaji.
- Alphonse Shija MAHUYEMBA

Soma zaidi hapa (kitabu) Mitishamba ya kutibia mimea na mifugo

Waionaje makala hii (Maoni)
Sahili__ni rahisi na inaeleweka
Tata__ ni ngumu kueleweka
Nzuri__inafaa kwa ajili ya wanadamu
Maoni kwa ufupi

_ Uk. Ufuatao

Taarifa zilizo katika mtandao huu hazilengi kuwa mbadala wa taarifa rasmi kutoka katika vyombo vyenye mamlaka kama, daktari au mtoa huduma ya afya. Au sekta yoyote rasmi. Taarifa na habari hizi ni kwa ajili ya ujuzi tu.